top of page
Search

Wajibu Wa Kina Mama Kukabiliana Na Misimamo Mikali Ya Matumizi Ya Nguvu | Citizen Support Mechanism


Mchango wa mama katika malezi ya mwana ni muhimu na hudhihirika mtoto anavyozidi kukua kiumri. Wasemavyo wahenga, mtoto umleavyo ndivyo akuavyo, mienendo ya mtoto anapokuwa mkubwa ni dhihirisho ya malezi aliyoyapata enzi za udogo wake. Hivyo basi, sharti akina mama ambao ni nguzo kuu katika ulezi washirikishwe katika viwango vyote vya malezi ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazowakumba watoto hususan katika ujana wao.


Mama ni chombo muhimu katika ukuzaji wa vizazi vichanga

Kila kuchapo, magenge ya kigaidi yenye nia ya kueneza fikra za kimageuzi yanazidi kuibuka, lengo lao kuu likiwa ni kufunza itikadi kali, kutia kasumba na kuwasajili vijana wengi kwenye makundi yenye misimamo mikali inayotumia nguvu. Sharti walezi wafahamu kuwa vijana wengi wamo katika hatari ya kuhadaiwa na makundi haya yenye misimamo mikali kutokana na shinikizo la wenzao, hali ngumu kiuchumi na utambulishaji, ili kuwaonya wakiwa wangali wachanga dhidi ya magenge hatari.


Kama nguzo kuu ya familia, akina mama hawana budi kushiriki katika vita dhidi ya ugaidi na ukinzaji fikra za kimageuzi zinazoibua misimamo mikali si nyumbani tu bali pia katika uongozi wa kitaifa. Licha ya kuwa wazazi wote -baba na mama wana majukumu ya kukuza watoto katika njia zinazofaa, aghalabu mama huwa karibu na watoto kwa muda mwingi na ni muhimu awajibike katika nidhamu na shughli zote azifanyazo mtoto ili kutoa mwelekeo na kuzuia visababishi vya kujiunga na makundi ya kigaidi. Mama ni chombo muhimu katika ukuzaji wa vizazi vichanga, sharti wamama wote wasimame tisti na kukemea itikadi potovu zinazopelekea vijana wengi kusajiliwa katika makundi yenye misimamo mikali.

85 views

Comments


bottom of page